Utafiti tulioufanya 26-27 september2010 katika uwekezaji wa mazao ya nishati hai (Bio-fuel) unaofanywa kwenye ardhi yenye rutuba katika wilaya ya Kisarawe,kata za Marumbo na Kibuta, vijiji vya Marumbo, Muhaga, Palaka na Mtakayo umebaini kuwa wanavijiji walinyang’anywa ardhi yao na kupewa mwekezaji wa mazao ya nishati hai. Inasikitisha kuona mkulima aliyelima shamba na kupanda mazao ya kudumu kama vile miembe,mikorosho na minazi na ambapo ardhi ndio mtaji wake wa kuzalisha chakula akinyang’anywa.
Pamoja na kuwa na sheria ya ardhi ya vijiji no 5 ya mwaka 1999 inayotambua mwakijiji yeyote alie kalia ardhi na kuitumia kuwa anamiliki ardhi hiyo kihalali bado kuna uporaji wa ardhi unaofanywa na maafisa wa ardhi wa wilaya.
Kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya vijiji, halmashauri ya kijiji ina uwezo wa kujadili maombi yaliyowasilishwa ndani ya siku tisini na kutoa majibu. Lakini cha kushangaza wanakijiji hawakupata fursa ya kumjadili mwekezaji huyo wala hakuna barua ya maombi ya mwekezaji, isipokuwa habari walizopata wanakijiji ni kuwa wanachotakiwa kufanya ni kuandika muhtasari wa kukubali kumpa mwekezaji.
Wakitoa ushuhuda jinsi ardhi yao ilivyoporwa wanakijiji wa muhaga walisema afisa ardhi alifika kijijini hapo na bila kutupa muda wa kumjadili mwekezaji alituambia mnachotakiwa kufanya ni kuandika muktasari wa mkutano wa kijiji kwani kampuni hiyo inayotaka ardhi ni kwa manufaa ya taifa na hatukutakiwa kuchelewesha kuandika muhtasari huo kwani vijiji vya jirani walishapeleka muhtasari zao wilayani. Kwa vile mbunge wetu nae alikuwepo na ndio kioo cha jamii tulikubali kumpa mwekezaji huyo ardhi. Bila ya kuwepo kwa mkataba wowote wala fidia ya ardhi iliyochukuliwa na mwekezaji hoyo mpaka sasa hatujui ukubwa wa eneo alilochukua mwekezaji kwani wakati mwekezaji anapimiwa eneo sisi hatukushirikishwa kazi hiyo imefanywa na maafisa ardhi wapimaji. Mwekezaji alishatuambia ni marufuku kuingia kuokota kuni kwenye eneo tulilompa .
Inahuzunisha kusikia mtu mwenye dhamana ya kuwasaidia wanakijiji katika mambo ya ardhi akitumia kutoelewa kwa wanakijiji kama njia ya kuwanyang’anya ardhi yao yenye rutuba kwa manufaa ya kampuni za kutoka nje ya nchi.
Ardhi ni mtaji wa kwanza muhimu kwa mtu masikini kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini na njaa na kama mtaji huo atanyang’anywa basi ni dhahiri kuwa kutakuwepo na uongezeka la umasikini na njaa na kushindwa kufikia malengo ya millennia namba moja la kupunguza umasikini na njaa ifikapo mwaka 2015. Zuia uporaji wa ardhi saidia wazalishaji wadogo.
No comments:
Post a Comment